Tafsri


TOFAUTI KATI YA UKALIMANI NA TAFSIRI:

KINADHARIA NA KIVITENDO.

Kika makala hii tutaanza kueleza maana ya tafsiri na ukalimani. Sehemu ya pili tutaeleza vipengele vinavyotofautisha taaluma ya tafsiri na ukalimani.
Kwa kuanza na maana ya tafsiri. Wataalamu mbalimbali wanaeleza maana tafsiri kama ifuatavyo;
Kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2006) wanaeleza kuwa tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine. Woa wanatilia mkazo katika zoezi la uhawilishaji na kinachohawilishwa ni mawazo katika maandishi.
Pia Catford (1965) anaeleza kuwa, kutafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha mmoja yaani lugha chanzi na kuweka badala yake mawazo yanayolingana kutoka katika lugha nyingine yaani lugha lengwa. Hapa msisitizo upo katika matini zilizoandikwa na kuzingatia zaidi ujumbe au wazo lililopo katika matini chanzi lijitokeze vile vile katika matini lengwa. Mawazo haya hayawezi kuwa sawa kabisa na ya matini chanzi bali ni mawazo yanayolingana toka matini chanzi na matini lengwa, hii ni kutokana na sababu tofauti kama vile utamaduni, historia, kiisimu na mazingira.
Naye Newmark (1982) anaeleza kuwa tafsiri ni mchakato wa uhawilishaji wa maneno kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa.
Pia Nida na Taber (1969) wanaeleza kuwa tafsiri hujumuisha kuzalisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe vya asili vya lugha lengwa vinavyo karibiana zaidi na lugha chanzi kimaana na kimtindo. Wao wanatilia mkazo uzalishaji upya wa kwa kutumia visawe asili vinavyokaribiana na matini chanzi kimaana na kimtindo. Kutokana na maana hizi tunaweza kusema kuwa tafsiri hufanywa katika ujumbe uliopo katika maandishi, ni jaribio la kiuhawilishaji na wazo linalatafsiriwa huwa na visawe vinavyokaribiana na sio sawa kutokana na tofauti za kiisimu, kihistoria, kiutamaduni na mazingira.
Pia maana ya ukalimani umefasiriwa kama ifuatavyo;
Kwa mujibu wa Wanjala (2011) anaeleza kuwa, ukalimani ni kuhawilisha ujumbe uliopo katika mazungumzo pamoja na uamilifu wake kutoka lugha chasili hadi lugha lengwa kwa kuzingatia isimu utamaduni na muktadha wa jamii husika.
Hivyo tunaweza kusema kuwa ukalimani ni uhawilishaji wa taarifa au ujumbe kutoka kwa msemaji wa lugha chanzi kwenda katika lugha lengwa kwa njia ya mdomo au mazungumzo, kwa kuzingatia isimu ya lugha husika, utamaduni na muktadha katika jamii fulani.
Kinadharia na kivitendo taaluma ya tafsiri na  taaluma ya  ukalimani ni tofauti. Tofauti hizo zinajitokeza katika vipengele vifuatavyo;
Kwa kutumia kigezo cha maana; tafsiri ni taaluma ya uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia isimu, mukutadha na utamaduni. Lakini ukalimani ni taaluma inayohusika na uhawilishaji wa taarifa au wazo kutoka kwa msemaji wa lugha chanzi kwenda katika lugha lengwa kwa njia ya mdomo au mazungumzo kwa kuzingatia isimu, utamaduni na  muktadha wa jamii. Hapa tunaona tofauti kuwa taaluma ya tafsiri inahaulisha ujumbe katika maandishi na ukalimani unahaulisha ujumbe katika mazungumzo.
Kwa kutumia kigezo cha ukongwe; Taaluma ya tafsiri imeanza hivi karibuni mara baada ya majilio ya maandishi. Hii ina maana kwamba baada ya kuwepo kwa maandishi ndipo taaluma hii ya tafsiri ikaanza. Lakini ukalimani ni taaluma kongwe zaidi kwani mazungumzo yalianza kabla ya maandishi. Ukalimani ulianza baada ya maingiliano ya jamii ndipo haja ya kukalimani ikaanza hususani katika shughuli za biashara, dini na kadhalika ndipo ilipolazimu uwepo wa ukalimani katika jamii ili kukidhi mawasiliano.
Kwa kutumia kigezo cha hadhira; Katika taaluma ya tafsiri huwa na hadhira ambayo haishirikiana moja kwa moja katika mchakato wa tafsiri. Hadhira ya tafsiri husoma tu kazi iliyotafsiriwa. Lakini katika taaluma ya ukalimani huwa na hadhira hai inayoshirikiana katika mchakato mzima wa ukalimani. Hii ina maana kwamba hadhira huweza kuwasiliiana na mkalimani endapo hadhira inahitaji jambo la ziada. Mfano katika ukalimani wa mikutano au makongamano na ukalimani wa kijamii kama vile katika masuala ya afya, maji, ujenzi wa shule , imani/ dini nakadhalika hadhira hushirikiana na mkalimani moja kwa moja.
Kwa kutumia kigezo cha stadi kuu na muhimu za lugha; Taaluma ya tafsiri huhusisha stadi kuu nne za muhimu ambazo ni kusoma, kuandika, kusikiliza na kuzungumza. Mfasiri anatakiwa kuwa na ujuzi wa taaluma hii ili kufanikisha mchakato wa tafsiri kwa ufanisi. Lakini katika taaluma ya ukalimani huhusisha stadi kuu muhimu kama vile kusikiliza kutoka kwa msemaji wa lugha chanzi, na kuzungumza kwenda kwa wasikilizaji, na kutunza kumbukumbu.
Kwa kutumia kigezo cha muda; taaluma ya tafsiri huchukua muda mrefu kuhawilisha ujumbe kwani maandishi huhitaji maandalizi, hela na wakati wa kutosha ili kupata kazi iliyo bora zaidi. Lakini taaluma ya ukalimani huchukua muda mfupi mno wa kuhawilisha ujumbe yaani hapo kwa  papo. Mfano ukalimani wa mahakamani, ukalimani wa mikutanoni au kwenye makongamano, warisha na semina mkalimani, hukalimani mfululizo kuendana na msemaji wa lugha lugha chanzi.
Kwa kutumia kigezo cha mfumo wa lugha ; katika taaluma ya tafsiri hutumia mfumo wa lugha ya maandishi. Lakini katika taaluma ya ukalimani hutumia mfumo wa lugha ya mazungumzo. Mfano ukalimani mfululizo au andamizi ambapo mkalimani huzungumza sambamba na msemaji wa lugha  chanzi hivyo mkalimani hufanya kazi kwa haraka sana ili kuendana na kasi ya mzungumzaji kama mfumo wa lugha ulivyo.
Kwa kutumia kigezo cha uwasilishaji; taaluma ya tafsiri, mfasiri ananafasi ya kudurusu kazi aliyopewa na kuweza kuondoa na kurekebisha au kusahihisha makosa yaliyojitokeza katika tafsiri yake. Lakini katika taaluma ya ukalimani, mkalimani hana nafasi ya kudurusu hata kama kuna kosa lililojitokeza. Na mara nyingi ukalimani huwa na makosa ya kimatamshi, kisarufi na kiuteuzi wa maneno.
Kwa kutumia kigezo cha utunzaji wa kumbukumbu; Katika taaluma ya tafsiri huwa na kumbukumbu ya kudumu kwani mawazo au ujumbe huifadhiwa katika maadhishi. Lakini katika taaluma ya ukalimani kumbukumbu sio ya kudumu kwani huwa katika mazungumzo kinadharia na kivitendo.
Ingawa taaluma hizi mbili yaani taaluma ya ukalimani na taaluma ya tafsiri zinatofautiana kwa kiwango fulani kinadharia na kivitendo lakini taaluma hizi mbili zinafanana.
Vigezo vinavyofananisha taaluma hizi mbili ni hivi vifuatavyo;
Taaluma zote mbili hushughulika na uhawilishaji wa ujumbe kutoka katika lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Taaluma zote hulenga kufanikisha mchakato wa mawasiliano kati ya watu au jamii mbili au zaidi zinazotumia lugha tofauti.
Taaluma zote mbili huchangiana na kushirikiana katika mambo makuu manne muhimu ambayo ni mtoa ujumbe, ujumbe wenyewe, mhawilishaji ujumbe na mpokeaji ujumbe. Mchango wa kila kipengele ni muhimu katika taaluma zote mbili ili kukamilisha mchakato mzima wa tafsiri na ukalimani.
Kwa kutumia kigezo cha uendeshwaji; taaluma zote mbili huweza kuendeshwa kwa namna mbili, binadamu au mashine zinazotumiwa kuhawilisha ujumbe kutoka katika lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Hivyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa licha ya kufanana na kutofautiana kwa dhana au taaluma hizi mbili, mfasili na mkalimani hawana budi kuzingatia isimu yaani sarufi ya lugha husika, utamaduni, muktadha husika na hata historia ya jamii husika.
Marejeo.
Catford J.C. (1965) A Linguistic theory of Translation: OUP London.
Mwansoko, H.J.M. na wenzake (2006) Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu: TUKI
                         Dar es Salaam.
Newmark, P. (1988) A Textbook of Translaton. : Prentice Hall London.
Nida, A. E. na Charles, R. T. (1969) The Theory and Practice of Translation. The United
                       Bible Societies: Netherlands.
Wanjala S. F (2011) Misingi ya ukalimani na tafsiri; Serengeti Education publisher (T)
                      L.T.D. Mwanza Tanzania


CHANGAMOTO ZA KITAMADUNI KATI YA LUGHA CHANZI NA LUGHA LENGWA

Makala hii inasehemu kuu tatu; sehemu ya kwanza ni fasili ya tafsiri, utamaduni na vipengele vya kiisimu ambavyo vinaleta changamoto katika mchakato wa kutafsiri. Sehemu ya pili ni vipengele vya kiutamaduni vinavyosababisha changamoto katika shughuli ya kutafsiri. Sehemu ya tatu ni hitimisho.
Wataalamu mbalimbali wanaeleza tafsiri kama ifuatavyo;
Newmark (1988) na Mwansoko na wenzake (2006) wanaelekena sana katika fasili zao ambapo wanaeleza kuwa; tafsiri ni zoezi la kuhawilisha mawazo au maneno ya lugha chanzi kwenda lugha lengwa. Kwa upande wa Nida na Taber  (1969) wanatofautiana kidogo na mawazo ya wataalamu wenzake kwa kutueleza kuwa; kutafsiri hujumuisha kuzalisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe asilia vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi kimaana na kimtindo.
Kutokana fasili za wataalamu hawa tunaweza kutoa maana ya tafsiri kuwa; ni uhawilishaji wa mawazo yaleyale yaliyoandikwa katika matini chanzi kuyapeleka katika matini lengwa.
Pia maana ya utamaduni imefasiliwa na wataalamu kama ifuatavyo;
Newmark (1988) anaeleza kuwa; utamaduni ni mkusanyiko wa mila na desturi zote za jamii inayotumia lugha mahususi kama njia yake ya mawasiliano.
Ruhumbika (1978:261) anatofautiana na mawazo ya Newmark kueleza utamaduni kwa kupinga kwamba utamaduni wa binadamu si mila na desturi zake na mambo ya yake tu. Bali utamaduni ni jumla ya juhudi zote za jamii fulani katika kila kipengele cha maisha, katika umma wake, katika filosofia zake za maisha, mfumo wa sheria zake, mbinu zake za ulinzi na usalama wa nchi, taratibu za kuelimisha raia zake, taratibu zake za mgawanyo wa kazi za uzalishaji mali na mifumo ya ugawaji wa matunda ya kazi hizo na juhudi za kuiwezesha jamii isonge mbele.
Kwa upande wa tofauti za kiisimu ambazo ni changamoto katika shughuli ya kutafsiri hujidhihirisha katika vipengele vikuu vinne yaani maumbo sauti, maumbo ya maneno, miundo ya sentensi pamoja na maana.
Baada ya kueleza fasili ya tafsiri  na utamaduni pamoja na kuainisha  vipengele vya kiisimu ambavyo ni changamoto katika tafsiri. Tuangalie sehemu ya pili ambayo ni tofauti za kiutamaduni ni changamoto kwa wafasiri wote katika shughuli nzima ya tafsiri. Vipengele vya kiutamaduni vinavyosababisha changamoto hizo zimebainishwa na wataalamu kama ifuatavyo;
Nida (1964) akinukuliwa na Mwansoko na wenzake (2006:31) na Newmark (1988:95) visawe vya utamaduni wamevibainisha katika makundi matano yaani; ekolojia, violwa, mila na desturi, siasa na dini. Licha ya wataalamu hawa kubainisha katika makundi matano kwa ujumla tumeweza kubaini kwamba kipengele cha kisiasa kinajitegemea hakiwezi kuingizwa katika utamaduni na kipengele cha dini nacho kinaingia katika kipengele cha mila na desturi. Hivyo kutokana na mawazo haya vipengele vya kiutamaduni tumevibainisha katika makundi manne yaani; ekolojia, violwa na mila na desturi pamoja na semi kwa mujibu wa mawazo yetu Tukianza kueleza kipengele kimoja hadi kingine namna vilivyo na changamoto katika tafsiri kwa mfasiri au wafasiri.
Ekolojia; suala la tabia za kijiografia kwa kawaida zinaweza kutofautiana kati ya utamaduni wa jamii moja na nyingine. Hivyo kwa mfasiri ni ugumu sana kupata visawe mwafaka kwa maneno husika. Mfano lugha ya Kiswahili huzungumzwa zaidi katika nchi za joto hususani za Afrika Mashariki ambapo tunabainisha misimu minne ya mwaka yaani kiangazi, vuli, masika na kipupwe. Lakini Kiingereza huzungumzwa nchi za baridi hususani Uingereza wao hubainisha misimu minne pia ya mwaka summer, autumn, winter na spring. Lakini kwa waingereza;
         Summer ni kiangazi (lakini joto la kiangazi ni kali zaidi ya lile la
         Summer wanalolifahamu Waswahili)
         Winter-kipupwe (lakini baridi ya winter kwa Waingereza ni kali
         zaidi ya ile ya baridi ya kipupwe wanayoifahamu Waswahili)
Pia kuna michezo ambayo hufanyika sehemu zenye baridi ambayo kwa kawaida haiwezi kufanyika  nchi za joto kama hizi za Afrika Mashariki. Kwa mfano;
Skate-sketi (mchezo wa kusketi).
Ski-skii (mchezo wa kuskii).
Hivyo kwa mfasiri itamwia vigumu sana kupata visawe sahihi hususani anapofasiri matini ya kiingereza kuzipeleka Kiswahili. Kwa sababu vipindi kama hivyo hatuna na michezo hiyo haipo kwa hiyo kupata kisawe mwafaka kwa neno husika ni vigumu.
Violwa; kuhususha suala la uvumbuzi wa kisayansi na teknolojia kuingizwa katika nchi zetu zinazoendelea. Uvumbuzi na ubunifu huu umeathiri sana utamaduni wa lugha yetu ya Kiswahili na kusababisha wafasiri kushindwa kupata visawe mwafaka kwa baadhi ya maneno katika lugha ya Kiswahili. Badala yake kinachofanyika ni kutohoa maneno hayo kutoka katika lugha ya Kiingereza kwa kuyafanyia tu marekebisho ya kisarufi yanapoingizwa katika lugha yetu yaani ya kimatamshi na kimaumbo. Kwa mfano;
Kiingereza            Kiswahili
Radio                    redio
Chemical               chemikali
Telefax                  telefaksi,
Digital                  digitali
Software              softiwea
Hardware          hadiwea           
Mila na desturi; tofauti hizi inaweza kujidhihirisha kupitia ulaji, vinywaji, mavazi na imani (dini) baina ya utamaduni wa jamii moja na jamii nyingine. Hivyo basi tofauti hizo ni changamoto kubwa sana kwa mfasiri au kwa wafasiri wakati wa kutafsiri. Tukianza na;
Ulaji; utamaduni wa Waswahili wanamilo mikuu mitatu tu yaani kifungua kinywa, chakula cha mchana na chakula cha jioni. Lakini Waingereza wao wanamilo mikuu mitano yaani breakfast, lunch, high tea, dinner na supper. Kwa hiyo kwa mfasiri wa Kiswahili high tea ambayo ni chai nzito kwa kawaida ambayo hunywewa 11-12 jioni itampa ugumu kuifasiri. Kwani katika utamaduni wetu wa Waswahili hatuna chai ambayo watu wanakunywa wakati huu. Hata supper mlo wa usiku kwa kawaida mwepesi pia itamwia vigumu sana kwa wafasiri kupata visawe kwa sababu katika utamaduni wetu hatuna chakula ambacho huwa kinaliwa wakati huu.
Pia hata Wafaransa wanamlo ambao huliwa kabla ya “Lunch” uitwao “Appacative” mlo huu kwa utamaduni wa Waswahili haupo hivyo kwa mfasiri ni vigumu sana kupata kisawe chake kitakachofanyika ni kutumia mbinu ya ufafanuzi kuwafanya hadhira lengwa kuelewa nini kinachomaanishwa.
Hata upande wa matini za Kiswahili ambapo mfasiri anapofasiri matini ya Kiswahili kuipeleka katika lugha ya Kiingereza atashindwa kufasiri maneno ya vyakula kama vile; ugali na kande kwa sababu katika utamaduni wa Waingereza hakuna vyakula hivi atakachofanya mfasiri ni kutumia mbinu ya kuhawilisha maneno kama yalivyo kuyapeleka katika lugha lengwa au kutumia mbinu ya ufafanuzi.
Vinywaji; kwa upande wa vinywaji baridi vinavyonywewa katika utamaduni wa Waingereza vimekosa visawe katika utamaduni wetu wa Waswahili. Kwa hiyo kwa wafasiri ni changamoto kinachofanyika yanatoholewa na kufanyiwa mabadiliko ya kisarufi hususani ya kimatamshi na kimaumbo.
Kwa mfano;  Cognac-konyagi, Whisky-wiski, Beer -bia  .
Pia kwa matini ya Kiswahili kuipeleka Kiingereza kuna baadhi ya vinywaji vinavyopatikana katika utamaduni wa Waswahili lakini utamaduni wa Waingereza havipo.
 Kwa mfano;      Ulanzi ,Mbege, Chibuku, Gongo
Kwa hiyo upande wa mfasiri ni vigumu sana kupata visawe kwa maneno haya. Mfasiri anakichofanya ni kutumia mbinu ya kuyahawilisha kama yalivyo kuyapeleka katika matini lengwa.
Mavazi; upande wa mavazi ni changamoto vilevile kwa wafasiri wote hususani pale unapokutana na mavazi ambayo asilia yake ni utamaduni fulani mfano yale ya Waingereza ambayo yanatengenezwa katika nchi yao. Suala hili linajidhihirisha katika jamii zetu za Waswahili mavazi mengi yanatoka nchi za Magharibi. Kinachofanyika yanatoholewa na kuyafanyia mbadiliko kidogo ya kisarufi ambayo kama vile ya  kimatamshi na kimaumbo.
Kwa mfano;   Skirts-sketi, Jeans-jinsi, Pullovers-pulova
Pia kwa mavazi ambayo kwa asili hutengenezwa katika nchi zetu vigumu sana kupata visawe yakitumika katika matini za Kiswahili wakati wa kutafsiri, kwa sababu nguo hizi zipo tu katika utamaduni wetu wa Waswahili. Utamaduni wa nchi za wenzetu hazivaliwe na hazitengenezwi. Kwa hiyo wafasiri wanachokifanya ni kuyahawilisha kama yalivyo wakati wa kutafsiri au ktumia mbinu ya ufafanuzi kuwafanya hadhira lengwa kujua nini kinachomaanishwa.
 Kwa mfano;   Khanga,  Kiko, Kitenge
Dini; kwa wafasiri masuala ya dini pia ni changamoto kubwa sana, kwani baadhi ya maneno mfano yatumiwayo katika utamaduni wa Waingereza yanayotaja nyama kama vile nyama nguruwe
Pork-nyama ya nguruwe.
Harm-paja la nguruwe lililokolea chumvi na kukaushwa katika moshi.
Bacon-nyama ya nguruwe iliyotiwa chumvi au kutengenezwa
           isioze.
Ni vigumu sana kupata visawe vyake katika lugha ya Kiswahili kutokana na kwamba utamaduni wa Waswahili kuathiriwa kwa kiasi fulani utamaduni wa lugha  ya kiarabu ambayo waamini wake wengi ni waislamu. Wafasiri wanachokifanya ni kutumia mbinu ya kuyahawilisha maneno haya kama yalivyo na kuyapeleka katika matini lengwa.
Kwa mfano; Kadhi, Hijabu, Nikabu., Sheikh.
Semi ni tungo au kauli fupifipu za kisanaa zenye lugha ya mafumbo ambazo hukusudia kuleta mafunzo kwa jamii husika. Semi ni moja ya kipengele kigumu katika kufanya kazi ya kutafsiri. Hii ni kutokana na tofauti kati ya utamaduni wa jamii moja na nyingine. Semi hizi zinaweza zikatumika katika jamii moja na jamii nyingine zisitumike semi hizo. Kwa hiyo hujidhihirisha katika vipengele vyake. Kwa mfano;
Methali -     Ndondondo si chururu, chururu si ndondondo.
Nahau      -Mkono mrefu (mchoyo),  -Zunguka mbuyu (toa rushwa), -Amevaa miwani (amelewa)
Misimu -   Amejaa upepo (amekasirika), -Amenitoa upepo ( nimempa fedha)
Vitendawili- Kuku wangu anataga mibani (nanasi),  -Popo mbili zavuka mto (macho)
Misemo -   Mtu ni afya (kuzingatia usafi),  -Maji ni uhai (kulinda vyanzo vya maji).
Metheli za kiingereza kama vile
-Advance is least heeded when most needed. Maana yake when the problem is serious people often don’t follow the advice given.
-All cats are grey in the dark. Maana yake people are undistinguished until they have made a name.
-A bad tree does not yield good apples. Maana yake a bad parent does not raise good children.
Hivyo basi wafasiri wengi wanachokifanya ni kutafuta semi ambazo huwa zinakaribiana na zile za lugha lengwa kwa lengo la kufikisha ujumbe uliokusudiwa  kwa hadhira lengwa hali ambayo inaweza kupotosha maana halisi ya semi husika ya matini chanzi ambayo inafungamana na utamaduni husika.
Kwa ujumla suala la kufasiri semi ni changamoto kubwa kwani semi nyingi hufungamanishwa na utamaduni wa jamii husika. Hivyo ni vizuri kufanya utafiti wa kina kwa wafasiri wote kabla ya kufanya tafsiri kwa hadhira chanzi kwa lengo la kuepukana changamoto hizi kwa kiasi fulani.
Changamoto hizi namna zitakavyoepukwa na wafasiri katika shughuli nzima ya kutafsiri kama ifuatavyo;
Suala la msingi kwa mfasiri ni lazima afahamu fika utamaduni wa lugha lengwa; hii itamsaidia mfasiri au wafasiri kufanya kazi za kutafsiri kwa ufanisi. Sululisho hili ni kwa mujibu wa maoni ya Mwansoko na wenzake (2006:36). Kwa maelezo ya wataalamu hawa mfasiri itamlazimu kutafiti kiundani sana utamaduni wa lugha ambayo anashughulikia.
Mfasiri anapaswa awe na umulisi wa lugha chanzi na lugha lengwa; ili anapokosa visawe mwafaka aweze kutumia mbinu ya ufafanuzi ili kuweka wazi wazo lililopo katika matini chanzi anapolitafsiri katika matini lengwa kwa lengo la kumfanya mteja au hadhira lengwa waelewe nini kinachomaanishwa.
Wataalamu wamejaribu kupendekeza mbinu kadha za kuepukana na changamoto za kiutamaduni wakati wa kutafsiri kwa mfasiri kama vile;
Matumizi ya tafsiri huru; mfasiri awe na ubunifu wa kuunda visawe vipya vinavyokubalika na lugha lengwa, hii itamsaidia mfasiri kupata visawe vinavyoendana na lugha chanzi wakati wa kufanya kazi yake ya kutafsiri kwa matini ambayo anaishughulikia.
Kukopa maneno; ni mbinu nzuri zaidi kwa mfasiri wakati wa kukabiliana na vipengele vya kiutamaduni vya matini chanzi kwa kutumia visawe vinavyokaribiana au kufanana na vile vya matini lengwa ambavyo vinafahamika na wasomaji wa matini lengwa. Kwa kuzingatia sheria na kanuni za lugha lengwa kwa dhana zisizofahamika. Ukopaji huu upo wa aina mbili yaani wa moja kwa moja (uhawilishaji) yaani ambao unafanyika pasipo kubadili umbo lolote la neno la lugha chanzi.
                  Kwa mfano;    kiingereza   (data)       Kiswahili   (data)
                 Kiswahili      (ugali )      Kiingereza   (ugali)
Ukopaji wa kubadilisha umbo la matamshi na umbo la neno (utohoaji); ukopaji ambao kuna mabadiliko kidogo ya kisarufi kwenye maneno ambayo yamekopwa kutoka lugha chanzi au lugha nyingine ambako neno hilo limekopwa kama vile  ya kimatamshi na kimaumbo.
            Kwa mfano;    Kiingereza        (Account, Photo)       Kiswahili          (akaunti,  Foto)  
Matumizi ya tanbihi; mfasiri anatakiwa kutoa maelezo ya ufafanuzi wa kina zaidi kuhusu zile dhana ngumu ambazo zinakuwa vigumu kueleweka na hadhira lengwa au mteja, wakati aisomapo matini husika kila mwishoni mwa kila ukurasa. Pamoja na faharasa mwishoni mwa kazi yake ya tafsiri.
Hitimisho; mfasiri hana budi kuzingatia kwa makini kipengele cha utamaduni pindi afanyapo kazi ya kufasiri ili asiweze kuhuisha maana iliyomaanishwa katika matini chanzi. Wakati anafanyapo kazi ya kuifasiri matini ambazo zinafungamanishwa na utamaduni wa jamii fulani.
MAREJEO.
Mwansoko, H. J. M. na wenzake, (2006) Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu.
                         Dar es Salaam: TUKI.
Newmark, P. (1988) A Textbook of Translaton. London: Prentice Hall.
Nida, A. E. na C. R Taber, (1969) The Theory and Practice of Translation. London:
                         Prentice Hall.
 Ruhumbika, G. (1978) “Tafsiri za Kigeni katika Ukuzaji wa Fasihi ya Kiswahili” Makala
                          kwenye Semina za Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili Dar es Salaam.
                          Dar es Salaam: TUKI.


TATHIMINI YA MATINI ILI  KUTAMBUA UBORA NA UDHAIFU WAKE KATIKA TAFSIRI.

Tuanze  na maana ya matini kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali kama vile ;Wamitila (2003) ameeleza kuwa matini inaweza kueleezwa kama kifungu cha maandishi au usemi wa lugha. Huweza kuelezwa  kwa kuangalia maumbo  ya kazi yake.
Oxford dictionary (2000) inaeleza matini kuwa ni andiko au chapisho linalohusu maudhui zaidi kuliko fani. Kutokana na maana hii tunaweza kusema kuwa si matini zote huzingatia zaidi kipengele cha fani na kuacha maudhui bali zipo ambazo huweka usawa katika vipengele hivyo na nyingine kama za kisiasa na zile za kisayansi zinahusisha zaidi kipengele cha maudhui kuliko fani. Hivyo kutokana na fasili zilizotolewa na wataalamu tunaweza kufasili matini kuwa;
Ni wazo au mfululizo wa mawazo ambao unajitosheleza kimaana. Au matini yaweza  ni neno moja, kirai, kishazi, sentensi, aya, au kifungu cha habari ambacho kinajitosheleza kimaana chenye ujumbe au wazo linalojitosheleza.
Katika tafsiri tunafanya tathimini ili kujua ubora na upungufu wa tafsiri husika. Neno tathini wataalamu wanatueleza kama ifuatavyo:
Wamitila (2003) anaeleza kuwa; kimsingi tunapotaja tathmini kuhusina na kazi za kifasihi humanisha kupima ubora na udhaifu wa kazi inayohusika. Mhakiki anaweza kupima kazi hiyo kwa kuiangalia maudhui yake au muundo wake kwa ujumla.
Lakini kutathmini tafsiri ni zoezi la kupima kiwango cha ubora wa tafsiri husika kwa kutumia mbinu zilizokubalika. Hivyo tunavyofanya tathmini ya tafsiri tunaweza kupata makundi makuu manne. Makundi hayo ni kama yafuatayo;
·         Tafsri bora
·         Tafsiri tenge
·         Tafsiri finyu
·         Tafsiri pana.
Katika kufanya tathmini kuna aina kuu mbili za matini ambazo zinaweza kufanyiwa tathmini, matini hizo ni kama  zifuatazo;
Matini lengwa zilizo katika mchakato wa kutafsiriwa. Matini hizi ni zile ambazo hazijafikishwa kwa mteja. Katika matini hizi mfasiri anaweza kutathmini tafsiri yake kwa lengo la kuiboresha kabla ya kuipeleka kwa mteja.
Matini lengwa zilizo katika mikono mwa mteja. Matini hizi mfasiri hufanya tathmini kwa lengo la kutoa maoni ambayo yatamwezesha mfasiri kuboresha kazi nyingine atakazozifanya baadae au kama atatoa toleo jingine.
Katika kufanya tathmini,  tamthiliya hii ya “Black Hermit” iliyoandikwa na Ngugi wa Thiong’o (1968) na kutafsiriwa kama “Mtawa Mweusi” na East African Educational Publishers Ltd. (2008), tumetathmini kwa kuangalia vipengele vifuatavyo;
Sarufi; katika kipengele hiki tumeangalia uzingativu wa vipengele vya kisarufi kama vile upatanisho wa kisarufi na upotoshaji wa maana.
Jukumu la kwanza la mfasiri ni kuhakikisha kwamba anazingatia na kuhifadhi upatanisho wa kisarufi wa matini chanzi. Lakini wakati mwingine jukumu hili halitekelezeki mfano wafasiri wa tamthiliya ya “Black Hermit” iliyotafsiriwa kama “Mtawa Mweusi” hawajazingatia upatanisho wa kisarufi na kufanya matini ya tafsiri ipoteze ubora wake.
      Mfano : Matini chanzi:  sorting out beans spread  in a basin. (Uk 1)
                   Matini lengwa:  akichagua harage katika bakuli. (Uk1)
                   Matini chanzi: if this be a curse put upon me (uk4)
                   Matin lengwa: kama hili ndilo laana nililopewa…(uk4)
Katika tafsiri ya kiswahili neno la kiingereza “beans” limefasiriwa kama “harage” badala ya “maharage” na pia katika tungo ya kiingereza “if this be a curse put upon me” limetafsiriwa kama “kama hili ndilo laana nililopewa”badala ya “kama hii ndio laana” tungo hizi zimefanya kukosekana kwa upatanisho wa kisarufi katika matini lengwa.
Katika suala la maana yawezekana mfasiri akachagua maana isiyo sahihi kati ya maana nyingi zilizo katika lugha lengwa za neno katika lugha chanzi. Mfano
Matini chanzi:                                                             Matini lengwa
… in a basin (uk1)                                                  : …katika bakuli(uk1)
 …carrying                                                            …akichukua
Do without husband                                          siwezi kuishi bila mwanaume
I have tasted the pains of beating               nimeona maumivu ya mapigo.
Katika tafsiri ya Kiswahili neno la kiingereza “basin” limefasiriwa kama “bakuli” badala ya “beseni”, neno “carrying” limetafsiriwa kama “akichukua” badala ya “akibebelea”, neno “do” limetafsiwa kama “kuishi” badala ya “kufanya” na neno “tasted” limetafsiriwa kama “nimeona”  badala ya “nimeonja”. Uteuzi wa maana za  msamiati katika matini legwa umepotosha maana iliyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi.
Kipengele cha pili ni muundo; kipengele hiki kinahusu ulinganifu wa mpangilio kati ya matini chanzi na matini lengwa. Tamthiliya ya “Black Hermit” ambayo ni matini chanzi imetumia muundo sahihi wa tamthiliya ambapo majina ya wahusika yanatokea kushoto. Lakini matini lengwa ambayo imetafsiriwa kama “Mtawa Mweusi” wafasiri wameitafsiri kwa muundo wa filamu, ambapo majina ya wahusika yamejitokeza katikati ya maelezo ya wahusika hivyo kukiuka muundo wa matini chanzi.
Vipengele vingine ambavyo tunaweza kuvifanyia tathmini katika tafsiri hii ya “Mtawa Mweusi” ni kama vile udondoshaji, upunguzaji na uteuzi mbaya wa maneno.
Udondoshaji; wafasiri wa matini hii kuna baadhi ya maneno ambayo ni ya msingi kukamilisha wazo au habaha ya msanii au mwandishi hayajitokeza ambayo yalikuwapo katika matini chanzi. Kwa mfano;
                Matini chanzi:  This temptation harping on weak flesh (uk4)
                Matini lengwa; Jaribu hili linalirudia rudia mwili wangu (uk.5)
                                                                      
Neno “weak” ambalo lipo kwenye matini chanzi halijafasiriwa katika matini lengwa na lilipaswa kufasiriwe kama “dhaifu”.
Uongezaji; katika matini lengwa kuna baadhi ya misamiati imeongezwa na wafasiri wakati katika matini chanzi haijatokea.
Mfano;
Matini chanzi:  A woman without a child is not a woman.  Uk. 4             
Matini  lengwa:  Mwanamke bila mtoto si mwanamke timamu.   Uk 3
Neno “timamu” lililotumiwa na wafasiri wa matini lengwa halipo kabisa katika matini chanzi.
Uteuzi m’baya wa msamiati; katika tafsiri ya “Mtawa Mweusi” wafasiri wameteua na kutumia visawe ambavyo vimesababisha upotoshaji wa ujumbe katika matini lengwa. Mfano wa viswe hivyo ni pamoja na :
Matinichanzi:  Have seen sunrise and sunset. (pg. 3)
                        I have tested the pains of beating. (pg. 3)
                        Together with power of the tribe. (pg. 10)               
Matini  lengwa: Yameona  kuchomoza na kuingia kwa jua. (uk. 3)
                           Nimeona maumivu ya mapigo. (uk. 4)
                           Pamoja na nguvu ya taifa. (uk. 10)
Katika matini ya lengwa wafasiri wameteua na kutumia visawe visivyokubalika kulingana na visawe vilivyotumika katika matini chanzi. Wafasiri wametumia neno “I have tested” kama “nimeona” badala ya “nimeonja” pia neno “tribe” likafasiliwa kama “taifa”.
Katika kufanya tathmini hususani katika kazi hizi mbili za tamthiliya tafsiri iliyofanyika ina mapungufu katika kila kipengele ambavyo ni msingi kuvizingatia wakati wa kufanya tafsiri. Vipengele hivi vimewakumba wafasiri wa tamthiliya labda kutokana na sabau za kutofatiana kiutamaduni, ujuzi wa lugha hizi kwa wafasiri wenyewe.

Marejeo
East African Educational Publishers Ltd (2008) Mtawa Mweusi. Kenya: Sitima Printers   
                          Stationers Ltd
Ngugi wa Thing’o (1968) Black Hermit. Kampala-Uganda: East African Educational Publishers
                          Stationers Ltd
Oxford Dictionary (2010) Oxford Advanced Learner’s Dictionary of Current English.
                            New York: Oxford University Press.
Wamitila, K.W (2003) Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi-Kenya:Focus:
                          Publication Ltd.
      

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni