Jumatatu, 6 Mei 2013

ISIMU



FONIMU INAVYOWEZA KUVUKA MPAKA WA FONIMU NA KUINGIA           KATIKA FONIMU NYINGINE.

Dhana ya fonimu ni dhana ambayo imejadiliwa na wataalamu mbalimbali wakitumia mitazamo tofauti tofauti. Wataalamu wafuatao wameeleza maana ya fonimu:-

Massamba, (2004) anasema fonimu ni kipande kidogo kabisa katika mfumo wa sauti za lugha ambacho kina sifa pambanuzi  kuweza kukitofautisha na vipande vingine vya aina yake. Sauti pambanuzi katika mfumo wa lugha.
Massamba na wenzake, (2004) wanasema fonimu ni kitamkwa kilicho bainifu katika lugha fulani maalumu.
Mgullu, akimnukuu Jones, (1975) anaeleza kuwa Fonimu ni kundi la sauti katika lugha fulani, lenye sauti muhimu (phonemes) pamoja na sauti zinazohusiana na ambazo hutumiwa mahali peke katika muktadha maalumu.
Tunaweza kusema kuwa wataalamu hawa wametofautiana katika kuelezea dhana nzima ya fonimu, wakati Massamba (2004), anasema fonimu ni kipande kidogo kabisa katika mfumo wa sauti za lugha, Jones (1975) akinukuliwa na Mgullu anasema kuwa fonimu ni kundi la sauti katika lugha fulani.
Hivyo  tunaweza kusema kuwa fonimu kipashio kidogo cha kifonolojia kinachoweza kubadili maana ya neno katika lugha fulani (mahususi). Kwa mfano pata – baba.
Dhana ya fonimu kuvuka mipaka na kuingia katika fonimu nyingine ni pale fonimu fulani inapoliacha umbo lake la asilia na kuingia katika umbo jingine. Dhana hii imenukuliwa na Massamba (2010) kutoka kwa mtaalamu Bloch (1941).
Bloch (1941) anashawishi kwa kiasi kikubwa kuwa fonimu kuvuka mipaka ni tukio la kawaida katika lugha ya asili kutokana na ushahidi kuwa alofoni za fonimu moja zinaweza kutofautiana kwa kiasi kikubwa kifonetiki. Wakati mwingine zinakuwa na uhusiano na alofoni za fonimu nyingine tofauti na fonimu zilimotokea. Vile vile kifonetiki, sauti fulani inaweza kutokea kuwa katika fonimu mbili au zaidi katika lugha moja.  Anaendelea kusema kuwa kuna aina mbili za fonimu kuvuka mipaka ambazo ni:-
Uvukaji mipaka usiokamili, unaamanisha hali ya fonimu ya aina moja kutokea katika fonimu mbili katika mazingira ya hali tofauti.
Kwa mfano;
Sauti [x] inaweza ikawa /a/ katika mazingira fulani na sauti [x] katika mazingira tofauti inaweza ikawa /b/, katika lugha ya Kidenimaki ( Jakoboson, Fant na Halle 1952) fonimu /t/ na /d/ zinakuwa na tabia tofauti mwishoni mwa silabi /t/ kutamkwa kama /d/ zinakuwa na mfano /hat/ kwenda /had/ wakati fonimu /d/ inakuwa / ð / . Kwa  mfano /had/ inakuwa /hað/ japokuwa katika Kidenimaki neno roof (paa) ni sawa sawa na tag wakati day (siku) ni dag. Hii inamaanisha kwamba mwanzoni mwa silabi fonimu /t/ na /d/ hazibadiliki. Kwa maana nyingine kuna /d/ inayotokana na /t/ pia kuna /d/inayotokana na /d/ yenyewe. 
Katika lugha ya Kiswahili uvukaji wa mipaka usiokamili wa fonimu hutokea katika hali zifuatazo:-
Kwa mfano:
 Udogo                          Ulimi                              Loa
Undugu                         Ndimi                      Ndoana
Ndugu
Hivyo katika Kiswahili sauti /d/ hujitokeza kama /d/ wakati mwingine huvuka mipaka na kuwa /l/. Sauti /l/ huwa /d/ endapo inatanguliwa na nazali /n/. Endapo tutajikita kifonetiki ni ngumu kutabiri /d/ kama ni alofoni ya fonimu /d/ au fonimu /l/ itakuwa rahisi.
Mfano mwingine wa Kiswahili ni pale:
Ki + ti  = ki+eusi (kiti cheusi) katika mifano ya Kiswahili tutaona mabadiliko ya kifonimu yakijitokeza katika mfano wa fonimu /k/ inapofuatiwa na irabu halafu kuwa katika mpaka wa mofimu kisha ikafuatiwa na irabu /e/ hubadilika na kuwa /ch/ yaani (ki+eusi) = cheusi.
Mfano mwingine katika Kiswahili ni:-
N + buzi  (mbuzi)  /n/ inakuwa /m/ ikifuatiwa na /b/
N+dama  (ndama)   /n/ inabakia kuwa /n/ ikifuatiwa na /d/
N+gombe (ng’ombe)  /n/ inabadilika na kuwa /n’g/
Pia tunaona kuwa nazali /n/ inapofuatiwa na kitamkwa /b/ hubadilika na kuwa /m/ inapofuatiwa na kitamkwa /d/ hubakia kuwa /n/ inapofuatiwa na kitamkwa /g/ hubadilika na kuwa [ ŋ ]. Hii inamaana kuwa katika mazingira haya sauti /m/, /n/ na [ŋ] ni alofoni za fonimu /N/
Uvukaji wa mipaka uliokamili. Huu ni uvukaji wa mipaka wa sauti moja kwenda sauti nyingine katika mazingira ya aina moja.
Kwa mfano:-
Katika lugha ya kiingereza uvukaji wa mipaka uliokamili unahusisha fonimu /t/ na /d/ inapotokea katikati ya irabu. Wamarekani hutamka sawa sauti ya ufizi [d].
Mfano:- Butter, Betting, Kitty ukiyatofautisha na Budden, Bedding, Kiddy katika mifano yote hiyo fonimu /t/ na /d/ hutamkwa sawa.
Kwa mfano:- /betting/ - [ beDiŋ] na /bedding/ = [beDiŋ]. Unapotamka haya maneno hautamki moja kwa moja /d/ wala /t/ bali inakuwa sauti katikati ya /t/ na /d/. Kwa msingi huo fonimu /t/  na /d/ hupoteza uhalisia wake katika matamshi. Baada ya ule uhalisia kupotea sauti inayokuja huziwakilisha haizitofautishi sauti  /t/ na /d/. aina hii ya uvukaji ndio huitwa uvukaji wa mipaka wa fonimu uliokamili.
Kutokana na mifano tajwa hapo juu ni dhahiri kuwa fonimu inaweza kutokea katika umbo lake asilia na kwenda katika umbo jingine la fonimu au alofoni ambazo hutokana na fonimu moja. Hii husababishwa na mazingira ya utokeaji wake au sifa za kifonolojia.
MAREJEO:

Massamba, D.P.B. (2004). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Taaasisi ya
                  Uchunguzi wa Kiswahili. Dar es salaam.
Massamba, D.P.B na wenzake. (2004). Fonolojia ya Kiswahili Sanifu. Taasisi ya
   Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Massamba, D.P.B. (2010). Phonological Theory: History and development.
   TUKI. Dar es saalam.